Dkt. Mpango : Viongozi wa mikoa kuweni picha ya mfano kwa wengine

0
260

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewataka Wakuu wa mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa mikoa kuzingatia maadili na nidhamu katika maeneo yao ya kazi ili kuwa picha nzuri na ya mfano kwa wengine.

Makamu wa Rais amesema hayo Kibaha mkoani Pwani alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere.

Amesema ni lazima wakati wote wa uongozi kutafuta njia bora ya kuwashirikisha wengine ili msingi wa uongozi na utendaji uwe chachu zaidi kuleta maendeleo kwa Wananchi.

Pia Makamu wa Rais amewataka viongozi hao wa mikoa kuongeza jitihada kuiwezesha sekta binafsi iweze kukua, kushamiri na kuzalisha ajira kwa kuweka vivutio na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Amesema sekta binafsi inapaswa kuwa mshirika muhimu katika shughuli zote za maendeleo katika mikoa.