Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watoaji wa huduma za kifedha nchini kutazama upya masharti ya mikopo ikiwemo dhamana ya mali zisizohamishika kwa kuwa ni kikwazo kwa wajasiriamali.
Pia amewataka kutafuta njia za kibunifu katika kuwafikia vijana nchini, ili waweze kupata mikopo itakayoinua maisha yao na uchumi wa Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo jijini Mwanza wakati akifungua maadhimisho ya pili ya wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa.
Amesema riba ya mikopo ya wastani wa asilimia 16 bado ni mzigo kwa Watanzania wengi, hivyo amesisitiza kila benki kupitia umoja wao kuchambua mizizi ya changamoto hiyo na kupunguza zaidi riba kwa wakopaji.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa wito kwa watoaji huduma za kifedha nchini kupunguza gharama za kutuma na kupokea pesa kimataifa kwa kuwa zimekuwa zikisababisha wageni pamoja na Diaspora kutumia njia zisizo rasmi.
Pia ameutaka Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kusaidia kuhamasisha wanachama wao kutanua wigo wa huduma za kifedha katika maeneo ya vijijini.