Dkt. Mpango azindua viwanda viwili Zanzibar

0
176

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo tarehe 8 Januari 2022 amezindua Viwanda vya Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) eneo la Mtoni KVZ Wilaya ya Magharibi A Unguja.

Viwanda vilivyozinduliwa na Makamu wa Rais ni kiwanda cha ushonaji na kiwanda cha Viatu.

Uzinduzi wa Viwanda hivyo ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya kuzindua viwanda hivyo, Makamu wa Rais amesema serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimedhamiria, pamoja na mambo mengine, kuimarisha sekta ya viwanda ili kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa na kuongeza ajira.

Amesema Kwa upande wa Tanzania Bara Serikali imedhamiria kujenga uchumi shindani wa viwanda ili kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati cha juu huku Dhamira hiyo ikienda sawia na azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukuza na kuvutia uwekezaji hususan katika viwanda ili kutimiza ile dhana ya Uchumi wa Buluu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Massoud Ali Mohammed amesema pamoja na kuongeza ajira lakini pia kiwanda hicho kimeondoa changamoto ya muda mrefu iliopata serikali katika kuagiza viatu na sare za Askari kutoka nje ya nchi.