Makamu wa Rais ametoa wito kwa wadau na taasisi kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Watoto Njiti).
Amesema wakati Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha huduma za watoto njiti, bado kuna vituo vya kutolea huduma za afya vina upungufu wa vifaa tiba vya kusaidia watoto hao pamoja na kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi husasani katika maeneo ya vijijini.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa kuhitimisha mbio maalum kwa ajili ya kusaidia watoto wenye magojwa ya moyo na wakina Mama wenye ujauzito hatarishi za CRDB zilizofanyika jijini Dar es salaam leo tarehe 14 Agosti 2022.
Kwa upande Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema Benki hiyo inatambua wajibu ilionao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya watanzania na hivyo kushirikiana na serikali na kuwekeza katika masuala ya jamii ikiwemo afya, elimu, mazingira na uwekezaji kwa wanawake na vijana.
Amesema mafanikio yaliopatikana katika mbio hizo mwaka 2020 yalipelekea mbio za Benki ya CRDB kutambulika kimataifa na shirikisho la kimataifa la mchezo wa riadha ambayo imetoa heshima kwa taifa.
Mbio hizo zimeshirikisha Viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete, Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu, Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango, Waziri wa Habari , Vijana ,Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Tabia Mwita Maulid, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Pauline Gekuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala, viongozi wa kampuni na taasisi mbalimbali pamoja na wananchi.