Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha miundombinu ya afya kwa kufanya matengenezo na kujenga miundombinu ya kisasa na kusogeza huduma ya afya karibu na wananchi huku mfumo wa rufaa ukiboreshwa zaidi.
Amesema hayo wakati akifungua Kituo cha Afya Daraja la Pili cha Kendwa kilichopo Wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Kituo hicho kitahudumia Shehia ya Kendwa, Kiwani, Mtangani na shehia nyingine za jirani na kuwezesha wananchi kupata huduma bora za matibabu ikiwa ni pamoja na huduma za mama na mtoto, maabara na huduma za chanjo pamoja na kusaidia kuwapunguzia wananchi hususani kinamama wajawazito kutembea masafa marefu kufuata huduma za afya.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa wananchi pamoja na watoa huduma katika kituo hicho kutunza vyema majengo na vifaa vilivyomo na vitakavyonunuliwa ili kuepusha gharama za matengenezo yasiyo ya lazima na kuwakumbusha viongozi wa kituo hicho kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha wanapanda miti katika eneo la Kituo pamoja na makazi ya madaktari na kutunza na kupendezesha mazingira yake kwa kuyaweka safi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh amesema wizara itaendelea kuhakikisha huduma zinazotolewa katika sekta ya afya zinaendana na wakati ikiwemo kuongeza vifaa mbalimbali vya kisasa katika maeneo ya kutolea huduma za afya.