Dkt. Kijaji aingia na ‘gear’ hii Wizara ya Habari

0
198

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji ameitaka menejimenti na watumishi wa wizara yake kutambua dhumuni kuu la wizara hiyo ni kuwatumikia wananchi.

Dkt. Kijaji amesema hayo katika kikao chake cha kwanza na menejimenti ya wizara katika ofisi za wizara, Dodoma mara baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino.

Amesema kuwa watendaji wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa sababu umma wa Watanzania una uchu wa kusikia kinachoendelea duniani hivyo kabla ya kufungia chombo chochote cha habari ni vyema kutekeleza wajibu kwanza.

“Mifumo yote ya Taifa hili ipo chini ya wizara hii na tumeunganishwa na Sekta ya Habari, twendeni tukahakikishe tunafanya kazi kwa matokeo yanayoonekana,” amesema Dkt. Kijaji.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa maelekezo aliyoyatoa waziri wake yamelenga kufanya kazi kwa matokeo yanayohitajika ili yalete mabadiliko katika jamii wanayoitumikia na kuahidi kuwa yeye binafsi pamoja na menejimenti wamepokea maelekezo hayo na watayafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo, Gerson Msigwa kwa niaba ya Menejimenti hiyo amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Waziri Kijaji na kuahidi kuwa watii, wasikivu na kuchapa kazi kwa kiwango kikubwa