Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameagiza kusimamishwa kazi kwa Meneja wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Kinyerezi I, Ubungo I pamoja na Mhandisi Mkuu wa Kinyerezi II, Kinyerezi I, na Ubungo I, ili kupisha uchunguzi dhidi yao kutoka na uzembe kazini.
Dkt. Kalemani ametoa maagizo hayo, wakati wa ziara yake ya kukagua vituo hivyo na baadaye kuzungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Februari 06, Jijini Dar es Salaam.
Aidha Dkt. Kalemani ametoa siku kumi na nne (14) kwa Bodi hiyo kuwafanyia uchunguzi mameneja na wahandisi wakuu hao na kumpatia majibu stahiki.
Dkt. Kalemani amesema kuwa, amefanya maamuzi hayo baada ya kubaini uzembe uliofanyika katika vituo hivyo, ikiwemo kutokuwepo kazini kwa watendaji hao na kutowajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.
“Haiwezekani Meneja na Mhandisi Mkuu wote wasiwepo katika vituo vyenu vya kazi bila sababu za msingi, mitambo yote inafanyiwa ukarabati kwa wakati mmoja, Hapana, hii haiwezekani ni uzembe wa hali ya juu lazima wachunguze na waondoke katika nafasi zao za kazi hawa watu wasije kutuletea matatizo, amesema Dkt. Kalemani.
Aidha aliiagiza Bodi ya TANESCO, kuhakikisha kuwa, mtaalamu wa kuunga kifaa cha kubusti umeme kilichopata hitilafu katika Kituo cha Kupoza umeme cha Kinyerenzi I, anapatikana na kufunga kifaa hicho ndani ya siku tatu (3) kuanzia leo na kituo hicho kizalishe umeme kama ilivyokuwa hapo awali.
Vilevile Waziri Kalemani ameitataka Bodi hiyo kufanya ukaguzi katika vituo vya kupoza na kusambaza umeme ili kuona hali halisi ya uzalishaji wa umeme katika mitambo yote, na ndani ya kipindi cha miezi miwili (2) mitambo yote tisa (9) iwe inafanya kazi kwa ufanisi.