Dkt. Biteko ataka Wazawa wapewe kipaumbe mradi wa bomba la mafuta

0
261

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewataka Watendaji katika kampuni inayotekeleza mradi wa bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kuhakikisha Watanzania wanapewa kipaumbele katika hatua zote za utekelezaji wa mradi huo.

Dkt. Biteko amesema hayo mara baada ya kufanya ziara katika kata ya Chongoleani jijini Tanga na kujionea kazi mbalimbali za ujenzi wa miundombinu katika eneo hilo ambalo mafuta kutoka nchini Uganda yatakuwa yakipokelewa na kuhifadhiwa.

“Serikali inataka kuona Watanzania wengi zaidi wanapewa kipaumbele cha ajira katika hatua zote za mradi na hii inajumuisha kampuni za Watanzania zinazotoa huduma mbalimbali, kwa kada ambazo ujuzi wake unapatikana ndani ya nchi Watanzania wapatiwe nafasi na kwa kada ambazo zinahitaji wataalam wa nje lazima kuwe na uwiano wa malipo kati ya Wazawa na wageni.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Kuhusu ujuzi unaotolewa na kampuni ya EACOP kwa Watanzania wakiwemo kutoka vijiji vinavyozunguka mradi, Dkt. Biteko ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha inatoa ujuzi ambao ni endelevu utakaowawezesha kuendelea na kazi hata pale mradi utakapokamilika.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo wa Bomba la Mafuta Ghafi litakalokuwa na urefu wa kilomita 1,443 Dkt. Biteko amesema kuwa unaendelea vizuiri na sasa umefikia asilimia 32 na mabomba yatakayopitisha mafuta yanaendelea kuingia nchini kwa ajili ya kuwekewa mifumo ya upashaji joto na plastiki itakayozuia upotevu wa joto kwenye mabomba hayo.