Dkt. Bashiru: Maalim Seif alikuwa kiungo muhimu kwa mafanikio ya Zanzibar

0
175

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amesema kifo cha Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kitaacha pengo kubwa visiwani humo.

Akizungumza n TBC, Dkt. Bashiru amesema Maalim Seif alikuwa kiungo muhimu sana kwenye serikali hasa katika siku 100 tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Nane.

“Maalim Seif alikuwa kiongozi shupavu na amekuwa kiongozi kwa nafasi mbalimbali akiwatumikia wananchi wa Zanzibar hivyo huu msiba umegusa wengi hasa ukiangalia siku 100 za uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi amefanyika kuwa kiungo muhimu kwa mafanikio ya serikali hii ya awamu ya nane,” amesema Dkt. Bashiru

Maalim Seif ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo amefariki dunia leo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia leo Februari 17, 2021.