Dkt. Bana: Tuna imani kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan

0
210

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Dkt. Benson Bana amesema mambo yaliyofanywa na aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Magufuli ni makubwa, lakini anaamini Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea pale alipoishia mtangulizi wake.

Dkt Bana ameyasema hayo mkoani Dar es salaam wakati wa mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)

Dkt. Bana ambaye kabla ya kuwa Balozi alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa, wakati wa uhai wake Dkt. Magufuli alifanya mambo makubwa ambayo hayana mfano Barani Afrika na hata katika mabara mengine.

Ameongeza kuwa Rais Samia Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mahiri, mwadilifu, mwenye uchungu na nchi yake na mwenye uzoefu wa kutosha, hivyo ni dhahiri kuwa atalivusha Taifa vema akifuata nyayo za Dkt. Magufuli.

Kuhusu uhusiano wa Tanzania na nchi za Afrika Magharibi ambako yeye pia ndiye Mwakilishi, Dkt. Bana amesema kwa upande wa Nigeria kazi kubwa iliyofanyika ni kuwashawishi Raia wa nchi hiyo wenye mitaji kuweza kuwekeza Tanzania.

Amezema Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria unaeendelea na kazi kubwa ya kutafuta Wawekezaji na kwamba mpaka sasa kuna kampuni kubwa tano za nchini humo zilizowekeza Tanzania ikiwemo ile ya Dangote.