Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, ametoa medali mbalimbali jijini Arusha leo Jumamosi, Oktoba 9, 2021, kwenye kilele cha Michezo ya Riadha Kitaifa, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina jambo na sekta ya michezo.
“Rais Samia ana jambo katika sekta ya michezo. Serikali yake inawekeza sana katika michezo kama sekta ya kimkakati kiuchumi, afya na utalii. Ndio maana ameongeza fedha za timu za Taifa, ametoa asilimia 5 ya mapato ya michezo ya kubashiri matokeo kusaidia michezo na mwaka huu tunakwenda kurejesha Taifa Cup ambapo michezo itachezwa kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa na kuja kitaifa. Uwekezaji huu umeanza kuleta tija michezoni. Tuwe wamoja tu,” alisema Dkt. Abbasi.
Ametumia fursa hiyo pia kuzitakia kheri na kuzipongeza timu mbalimbali za Tanzania ambazo zinacheza/zimetwaa ubingwa wa aina mbalimbali; Twiga Stars na Tanzanite Ladies (U20) leo zinashuka dimbani Twiga ikiwania ubingwa katika fainali za COSAFA kule Afrika Kusini na Tanzanite ikicheza na Eritrea Dar kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia.
Ameitakia kheri Taifa Stars inayoshuka uwanjani kesho nchini Benin na ameipongeza Timu ya Taifa ya Kriketi U19 ambayo imeshika nafasi ya tatu Afrika katika mashindano ya Afrika yaliyomalizika juzi nchini Rwanda.