Dkt Abbasi : Msikandamize Wasanii, muwasaidie

0
140

Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amezitaka taasisi za sanaa nchini kuendeleza sanaa, na sio kuwa chombo cha kuonea na kukandamiza Wasanii.

Dkt. Abbasi amesema hayo mkoani Dar es salaam wakati wa hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Elimu ya Masoko na Mabadiliko ya Matumizi ya Kidigitali kwa Kazi za Muziki nchini, iliyoandaliwa na kampuni ya Transsnet MusicTanzania.

“Taasisi zetu zinatakiwa ziwe sehemu ya kukuza sanaa na si kugeuka kuwa polisi ama mgambo, tuzitangaze kazi za sanaa na tuwasaidie Wasanii wetu kukua badala ya kuwakandamiza.” amesema Dkt. Abbasi.

Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa Wasanii kufanya kazi bora zaidi kwani jamii imeikubali sanaa, Wasanii watumie vipaji vyao na ubunifu kufanya kazi bora na kujifunza namna ya kuuza kazi hizo kwa kutumia njia za kisasa kama Boomplay.

Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na Wasanii kuboresha kazi zao, na pia kuhakikisha wanapata namna tofauti za kuuza kazi zao kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Boomplay Tanzania, Natasha Stambuli amesema wako tayari kushirikiana na Serikali kukuza sekta ya sanaa nchini, kwa kuwawezesha Wasanii kuuza kazi zao kwa njia ya mtandao.