Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Hassan Abbasi amesema kuwa, Serikali itaendelea kuliboresha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ili liendelee kuwahudumia Wananchi kwa viwango bora zaidi.
Dkt Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali amesema hayo leo wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TBC jijini Dar es Salaam, na kutumia jukwaa hilo kutoa nasaha zake kwa shirika.
Amesema kuwa kuna mambo sita ya msingi ambayo TBC na Watumishi wake wanatakiwa kuzingatia wakati ikianza mwaka 2021 ili waweze kufanya kazi kwa viwango ambavyo Wananchi na Serikali inatarajia.
Amesema kwanza ni kuwa na malengo yanayotekelezeka, kwani kuwa na malengo tu haitoshi, ni lazima ionekane wazi kuwa yanatekelezeka ili shirika liweze kupiga hatua.
Pili, amesema mbali na kuwa na mipango inayotekelezeka, lakini pia iwe mipango mikubwa kwani shirika na serikali zinauwezo wa kuitekeleza. Amesema ni bora mtu akawa na lengo kubwa mfano la kujenga ghorofa 100, hata ikitokea ameshindwa, atajenga 80 au 50.
Dkt Abbasi amewataka Wafanyakazi wa TBC wawe watekelezaji, ili mipango yao mikubwa na inayotekeleza isiishie kwenye karatasi.
Amesisitiza umuhimu wa kushirikiana huku akibainisha kuwa kila mmoja kwa nafasi yake ana umuhimu katika kufanikisha mipango ya shirika.
Kuhusu maadili kazini, amesema ni muhimu Wafanyakazi wakaacha uvivu, majungu, fitina na watimize wajibu wao na kwamba maadili ni pamoja na Watumishi kuwahi kazini na kuanza kazi kwa wakati.
Mbali na ahadi ya Serikali kuendelea kuiboresha TBC katika siku zijazo, Dkt Abbasi amesema kwa kipindi kilichopita Serikali imefanya mengi ikiwa ni pamoja na kuliongezea shirika hilo fedha za maendeleo, kuongezwa kwa Wafanyakazi ambapo wengine wamehamishwa kutoka idara mbalimbali na kutoa ajira mpya.