Dkt. Abbasi atoa siku 30 kuwasilishwa mikakati ya kuwainua wasanii nchini

0
340

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi ametoa siku 30 kwa viongozi wote wa vyama na mashirikisho ya sanaa nchini kuwasilisha mikakati ya mambo ambayo wanahitaji serikali iyaboreshe ili kuongeza tija kwa tasnia ya sanaa.

Dkt. Abbasi ametoa agizo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa viongozi wa vyama na mashirikisho ya sanaa pamoja na wachapishaji kilicholenga kuchambua mambo ambayo sekta ya sanaa inahitaji serikali iyafanye kutatua mahitaji mahususi ya kuendeleza sekta hiyo.

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anataka sekta ya sanaa iboreshwe ili wasanii waweze kunufaika na kazi zao hivyo ningependa kupata angalau mambo matano makubwa, ambayo mnaanini serikali ikiyafanyia kazi yatasaidia sekta hii kusonga mbele na kuleta mabadiliko chanya, ili tujenge hoja kama inavyofanyika katika sekta nyingine,”amesema Dkt. Abbasi.

Akiendelea kuzungumza amesema kumekuwepo na malalamiko mengi ya ukiukwaji wa katiba na kanuni za uendeshaji wa mashirikisho hayo hivyo amewataka viongozi wa vyama na mashirikisho kuzingatia utawala bora na kuacha migogoro kwani serikali haitaweza kufanya kazi na viongozi wenye migogoro.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa Tanzania, Godfrey Mngereza ametoa msisitizo kwa kamati iliyoundwa kufuatilia masoko ya kazi za sanaa, kufanya utafiti wa kina ili kubaini namna wasanii wanaweza kushiriki katika fursa za kitaifa na kimataifa.