Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la rufaa ili kutoa fursa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa kuwasilisha taarifa za uthibitisho ili kuongezewa viwango vya mikopo kulingana na uhitaji wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema dirisha hilo litakuwa wazi hadi tarehe 20 mwezi huu na kuwa rufaa kutoka kwa wanafunzi zinapaswa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao.
“Hadi leo [Novemba 13, 2022], tumeshawapangia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 na tunafahamu kuwa kuna wanafunzi ambao kwa sababu mbalimbali hawakukamilisha nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, dirisha la rufaa ni fursa kwao,” amesema Badru
Kwa mujibu wa Badru, lengo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 71, 000 katika mwaka wa masomo 2022/2023 na kuwasihi wanafunzi wanaowasilisha rufaa kusoma na kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mfumo wa kuwasilisha rufaa.
Taarifa ya HESLB imekuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia wanafunzi wote wenye sifa za kupata mikopo lakini hawakupata kupokelewa vyuoni na kusajiliwa ili kuendelea na masomo, ambapo wanafunzi 28,000 watanufaika na uamuzi huo.
Vyuo vimetakiwa kuwapokea na kuwasajili chini ya utaratibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.