Deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 71.559 hadi Juni 2022 kufuatia kupokelewa kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/2024.
Amesema deni la Serikali limeongezeka kutokana na kutolewa kwa hatifungani maalumu ya shilingi trilioni 2.17 kwa ajili ya kulipa deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) linalohusu michango ya watumishi waliokuwa kwenye utumishi kabla ya mwaka 1999.
Licha ya ongezeko hilo amesema Oktoba 7, 2022 kampuni ya Moody’s Investors Service ambayo ni mbobezi katika masuala ya kupima uhimilivu wa deni duniani walitoa taarifa inayoonesha kuwa mwelekeo wa hali ya uhimilivu wa deni la Tanzania umeimarika (positive outlook).
Serikali imesema inachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha deni linaendelea kuwa himilivu ikiwa ni pamoja na kuelekeza fedha za mikopo kwenye sekta za uzalishaji na miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na mauzo nje ya nchi na kutoa kipaumbele kwenye mikopo yenye masharti nafuu (semi concessional loans).
Hatua nyingine ni kuimarisha mikakati ya kukusanya mapato ya ndani ili kuhakikisha sehemu kubwa ya bajeti inagharamiwa na mapato ya ndani, kuweka mazingira rafiki ya kuvutia biashara na uwekezaji ili kuongeza fursa za kiuchumi (ajira, malighafi, kipato, mapato ya kodi) na kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya Serikali.