Mkuu wa wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Dkt. Philis Nyimbi, amefanya ukaguzi wa kushtukiza katika shule ya awali na msingi ya Bethania na kubaini kuwepo kwa mapungufu lukuki ikiwemo utata kwenye uhalali wa usajili wa shule hiyo.
Dkt.Nyimbi amesema shule hiyo inaonekana kusajiliwa katika wilaya ya Ilala ilihali ipo Nyamagana, huku baadhi ya walimu wakiwa hawana sifa na wengine kutoka nje na hawana vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
“Baadhi ya walimu hawana vibali, ndio maana nilivyoingia hapa wamekimbia, sasa nakuagiza kuwaleta walimu hao wawili na faili la kila mwalimu aliyepo hapo,” ameongeza Dkt. Nyimbi.
Mbali na utata wa usajili wa shule hiyo, pia miundombinu yake haikidhi mazingira ya utoaji wa elimu bora, hivyo kuagiza kurekebishwa kwa mapungufu yaliyobainika ndani ya muda wa mwezi mmoja.
Pia Dkt. Nyimbi amemuagiza mdhibiti mkuu ubora wa shule na afisa elimu msingi wilaya ya Nyamagana kuandaa ripoti ya shule hiyo.