DC Mbogwe ataka umakini ukusanyaji mapato

0
209

Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Sakina Mohammed amewataka watendaji wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato kufanya kazi hiyo kwa umakini na uadilifu.

Amesema ni jambo linaloshangaza mtendaji kukusanya shilingi elfu tatu hadi elfu tano kwa siku kwa kutumia mashine za kukusanyia mapato ya Serikali za Mitaa “POS”, wakati kuna uwezekano wa kukusanya mapato zaidi kutokana na eneo hilo kuwa na shughuli nyingi za kibiashara.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbogwe amesema hayo wakati wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe lililofanyika katika Kijiji cha Bwelwa na kuwataka watendaji wanaofanya hivyo kujitathmini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe, Saada Mwaruka amemuagiza Afisa Mapato hadi kufikia leo Mei 17, 2024 awe amekabidhi kwa watendaji wanaokusanya mapato mashine 23 za POS zilizobakia ofisini ili wakazifanyie kazi.