Daraja la Tanzanite kuanza kutumika Februari mosi

0
160

Daraja la Tanzanite linalopita juu ya Bahari ya Hindi limekamilika na litaanza kutumiwa na wakazi wa Dar es Salaam kuanzia Februari Mosi 2022, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema.

Daraja hilo linatarajiwa kupunguza msongamano wa magari katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barack Obama wakati wa kuingia na kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Daraja la zamani la Selander linapitisha zaidi ya magari 45,000 kwa siku, hivyo kukamilika daraja jipya kutasaidia sana kupunguza idadi ya magari yanayopita katika daraja la zamani la Selander na hivyo kuepusha kabisa msongamano wa foleni.

Mbali na foleni, pia litasaidia kukuza sekta ya utalii kwa sababu eneo hilo liko pembeni ya fukwe ya bahari ambapo watu wengi watakuwa wakienda kujivinjari.

Daraja hilo lina urefu wa kilometa 1.03, lina njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu na limejengwa pamoja na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2.