Daraja la Kigongo-Busisi, mfupa aliouweza Magufuli

0
449

Disemba 7, 2019 Rais wa Tanzania wakati huo, Marehemu Dkt. John Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Kigogo-Busisi ambalo ujenzi wake bado unaendelea.

Daraja hilo linalokatisha juu ya ziwa Victoria na kuunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema za mkoa wa Mwanza nchini Tanzania lina urefu wa kilomita 3.2 na litakapokamilika litakuwa ndilo daraja refu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mpango wa kujenga daraja hilo ulikuwepo tangu Serikali ya awamu ya kwanza lakini haukutekelezwa hadi Serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. Magufuli.

Wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa daraja hilo aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwele alisema kuwa ujenzi wake utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 700.

AIdha, mradi huo pia unahusisha ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.6.

Dkt. Magufuli alisema kukamilika kwa mradi huo siyo tu kutarahisisha usafiri na usafirishaji, bali pia utaondoa adha ya wagonjwa kupoteza maisha wakati wakisubiri vivuko vinavyotoa huduma katika eneo hilo.

Ujenzi wa mradi huo unaosubiriwa kwa hamu na Wananchi wa Mwanza, Geita na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo bado unaendelea.