Shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli inaendelea leo kwa mkoa wa Dar es salaam na ni siku ya mwisho kwa mkoa huo.
Hapo jana baadhi ya Viongozi pamoja na wakazi mbalimbali wa mkoa wa Dar es salaam walipata nafasi ya kuuaga mwili huo, shughuli inayofanyika katika uwanja wa Uhuru.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, -Aboubakar Kunenge amesema kwa mkoa wake shughuli hiyo itahitimishwa majira ya alasiri na baadaye mwili wa Dkt Magufuli utsafirishwa kuelekea mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na uongozi wa mkoa wa Dodoma, mwili wa Dkt Magufuli utawasili mkoani humo leo jioni na kulala Ikulu ya Chamwino.
Msafara utakaobeba mwili huo utapita katika barabara za Chako ni Chako, Nyerere, Bunge, Morena, Buigiri hadi Ikulu.
Kesho asubuhi utapelekwa katika uwanja wa Jamhuri kupitia barabara mpya ya Mfugale, Buigiri, Morena, Bunge, mzunguko wa mkuu wa mkoa pamoja na Nyerere na ndio.itakuwa shughuli ya kuuaga Kitaifa.
Watu mbalimbali kutoka ndani ya nje ya Tanzania, wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, watashiriki katika shughuli hiyo ya Kitaifa ya kumuaga Dkt Magufuli.