COSTEC yadhamini mkutano wa Elimu kwa Umma

0
99

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeelezea namna inavyofanya kazi zake mbele washitiri wa mkutano wa 106 wa mafunzo ya watayarishaji vipindi vya elimu kwa umma wa mwaka ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) uliofanyika kwa muda wa siku tano mkoani Iringa ambapo COSTECH ni mdhamini mkuu.

Akiwasilisha mada ya majukumu ya COSTECH, Dkt. Bunini Manyilizu ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa amesema kuwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ilianzishwa kutokana na sheria namba 7 ya mwaka 1986 na kuongeza kuwa Tume ilirasimishwa rasmi mwaka 1988 kama mrithi wa Baraza la Taifa la Utafiti.

Dkt. Bunini amefafanua kuwa kutokana na mamlaka ya kisheria ambayo Tume imekasimiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mshauri Mkuu wa Serikali kwa masuala yote yahusuyo Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini.

“COSTECH ina jumla ya kurugenzi nne ambazo mojawapo ni kurugenzi ya uratibu na uendelezaji wa Tafiti, kurugenzi ya Kituo cha Uendelezaji na uwasilishaji wa Teknolojia, kurugenzi ya Menejimenti ya maarifa na kurugenzi ya huduma za taasisi, Tume ina jukumu pia la kuwatambua watafiti na kuzisajili tafiti zote nchini pamoja na kutoa vibali vya utafiti nchini kwa wageni na watafiti wote nchini.” amesema Dkt. Bunini

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha ameishukuru Tume kwa ushirikiano wake wa kudhamini mkutano huo na kuongeza kuwa ili tafiti kupitia maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini zinapaswa kupewa kipaumbele hususani kwa nchi za Afrika kwa kuhakikisha zinapatiwa walau asilimia moja ya pato ghafi la Taifa (GDP) ili kurahisisha mchakato wa maendeleo kwa haraka zaidi.

Baadhi ya washitiri walioshiriki mkutano huo wa mafunzo ya watayarishaji vipindi vya elimu kwa umma wametoa maoni yao lengo likiwa ni kuhakikisha COSTECH inaongeza uhusiano wa karibu na wanataaluma wa habari na mawasilino ya umma ili kusaidia uchakataji wa taarifa za sayansi na teknolojia ziweze kuwafikia walengwa kwa lugha rahisi na inayoeleweka.