Corona: Tanzania yapokea msaada wa vifaa kinga kutoka China

0
510

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea msaada wa vifaa kinga vyenye thamani ya shilingi milioni 700.8 kutoka Serikali ya China.

Akipokea msaada huo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof. Mabula Mchembe amesema kwamba msaada huo umekuja wakati mzuri kwani utawasaidia watumishi wa afya katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19).

“Niwaombe na niwasisitize wafanyakazi wa afya, mjitahidi kuwahudumia watu wenye magonjwa mengine tofauti na ugonjwa wa Corona, huku mkiendelea kutekeleza wajibu wetu kwa wagonjwa wa Covid-19,” amesema Mchembe

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Gabriel Mhidze ameshukuru kwa kupatiwa msaada huo kutoka China na ameahidi kwamba utasambazwa kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.

“Nashukuru Serikali ya China kwa msaada huu, hivi sasa naweza kusema bohari yangu ina vifaa vya kutosha kusambaza kwa walengwa wote nchini,” amesema.

Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke amesema Serikali yake ya China imetoa barakoa 12,000, gloves 10,000, viatu 10,000 pamoja na vifaa kinga mbalimbali kwa ajili ya wataalamu wa afya.

“Kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na janga hili la ugonjwa Corona, ili kulinda maisha ya watu wake, napenda kusema kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika mapambano haya,” amesema Balozi Wang Ke.