Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari za kujikinga na UVIKO-19 hasa msimu huu wa sikukuu kwani ongezeko la wasafiri ni ishara kwamba kasi ya maambukizi nayo inaongezeka.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ametoa tahadhari hiyo wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango harakishi na shirikishi wa uchanjaji dhidi ya Corona yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Ngarenaro, Mkoani Arusha.
Waziri Gwajima ameeleza kuwa mpango huo unamlenga mwananchi kwa kuleta chanjo karibu kabisa na shughuli zao za kijamii ili kila mmoja aweze kuchanja bila vikwazo wala kumchelewesha katika majukumu yake ya kila siku.
Dkt. Gwajima ameelezea umuhimu wa kupata chanjo kwa mwananchi wa kawaida kwani kati ya watu 10 wanaofariki kutokana na UVIKO saba kati yao ni wasiochanja.
“Aliyechanjwa hata akiambukizwa ugonjwa unakuwa mwepesi sana tofauti na asiyechanja” amesisitiza Dkt. Gwajima
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, idara kuu ya afya Profesa Abel Makubi amewasihi wananchi kuzingatia njia zote za kujikinga na UVIKO ikiwemo kuchanja bila kusahau mazoezi ambayo ni muhimu kwa kuimarisha kingamwili.
Mikoa ya Ruvuma, Mwanza, kagera na Mara imetajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa idadi kubwa ya watu waliochanja.