Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amezitaka mamlaka mkoani Rukwa kusimamia kikamilifu sheria ya mazingira ya mwaka 2004 inayozuia shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi, ili kulinda barabara na madaraja katika bonde la mto Rukwa.
Mhandisi Kasekenya amesema hayo mara baada ya kukagua barabara ya Ntendo – Muze yenye urefu wa kilomita 37 na barabara ya Kasansa – Kilyamatundu yenye urefu wa kilomita 175 ambazo zimeathiriwa na mafuriko ya mvua kutokana na shughuli za kibinadamu za ukataji miti, kilimo na ufugaji katika safu za milima ya ukanda wa bonde hilo.
“Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji hakikisheni tabia ya uharibifu wa mazingira zinazofanywa na Wananchi zinakomeshwa mara moja ili kulinda hifadhi za misitu na miundombinu ya barabara na madaraja,”amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Amesema zaidi ya shilingi Bilioni 4.4 zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha barabara hizo zilizoko katika bonde la mto Rukwa ambalo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula zinakarabatiwa, ili kupitika wakati wote wa mwaka na kutoathiri uchumi wa Wakazi wa mkoa huo.
Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Rukwa Mhandisi Jotrevas August amesema kuwa, madaraja madogo 19 yamebomolewa na mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika ukanda huo na hivyo Wakala umejipanga kuhakikisha ujenzi wake unaendelea ili kutoathiri huduma ya usafiri katika barabara hizo.
Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.