Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amevitaka vikao mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea katika ngazi husika visisite kukata majina ya wagombea wanaofanya mbwembwe za kutembea na wafuasi wanapokwenda kuchukua fomu za kugombea kwani kufanya hivyo ni kuanza kampeni kabla ya wakati.
Ameongeza kuwa, hawawezi kuwa na chama ambacho kinatoa maelekezo kwa ajili ya kutoa fursa na haki sawa kwa wote kugombea nafasi mbalimbali wao wachache kuona wanapembe ndefu kuliko chama chenyewe, kwa kufanya wanayotaka alafu vikao viwapitishe.
Chongolo ameyasema hayo leo tarehe 13 Julai, 2022 wakati akifungua kongamano la Mafunzo ya Uongozi kwa mabalozi wa mashina na viongozi wa matawi mkoa wa Dodoma .
Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya wanachama kuanza kujipitisha katika majimbo kutafuta wapambe kwa kupanga safu katika Uchaguzi Mkuu wa ndani ya chama unaoendelea ili wawasaidia kwenye malengo yao ya Ubunge na udiwani kwa mwaka 2025.
Ameeleza kuwa, chama hakitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa taratibu, kanuni na katiba ya CCM ili kuwadhibiti watu hao, kwani muda wa uchaguzi bado na sasa kila jimbo lina mbunge na kila kata kuna diwani hivyo ni vema kwa kila mwanachama kusubiri muda ufike na sio kuanza sasa wakati viongozi waliochaguliwa wanafanya kazi ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi.