Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewaagiza Makatibu wa Wilaya maeneo yaliyobainika kuwa na kasoro ikiwemo baadhi ya watia nia kunyimwa fomu kwenye uchukuaji fomu ngazi ya shina nchi nzima kurudia zoezi hilo kwa sababu CCM sio chama cha mtu binafsi bali cha wanachama wote.
Maagizo hayo ameyatoa leo jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya ya Ubungo na Kinondoni.
“Nawaagiza makatibu wa wilaya zote nchini, maeneo yote ambayo tumebaini yana changamoto ya watu kunyimwa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, tunarudisha zoezi la kutoa fomu, tunataka wale wote wenye dhamira ya kuchukua fomu wachukue bila kuwekewa vizuizi, hiki sio chama cha mtu, hiki sio chama cha maslahi binafsi, hiki chama ni cha wanachama, na ni lazima tutende haki kwa kuwa katiba yetu ya CCM inatutaka tufanye hivo,” Katibu Mkuu ameeleza.
Ameongeza kuwa “Tunafuatilia na tukibaini kuna maeneo ambapo vitabu vilivyokuwa vimehakikiwa vimeongezwa majina ya watu wasiokuwemo kwenye utaratibu wa daftari la wanachama, Wakurugenzi/Makatibu wa uchaguzi watawajibika, hili sihitaji kusisitiza sana tutakutana baadaye na hili ni kwa ngazi zote.”
Ameyataja baadhi ya maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto hiyo kuwa ni pamoja na Wilaya ya Ubungo, Babati, Mbeya, Tabora na kusema ni lazima haki itendeke ndani ya chama kwa wanachama wote bila ubaguzi.
Pia Katibu Mkuu amewaasa vijana kuacha kuwa wapambe tu wa wagombea, nao wana haki ya kugombea.
“Acheni kubaki vijana wa hamasa tu ama wapambe wa wagombea, chukueni fomu gombeeni na mkiona kuna mazingira ya kuwafungia milango, tuambieni haraka sisi tuna funguo za kufungulia.”