Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Iringa Mhandisi Makoli Kisare, kutengeneza barabarani yenye urefu wa Kilomita moja ya kuelekea kituo cha afya Ifingo kata ya Kinyambo kuanzia kesho, ili kupunguza adha kwa Wananchi wanaokwenda kupata huduma katika kituo hicho.
Chongolo ametoa agizo hilo Mei 27, 2023 baada ya kukagua kituo cha afya Ifingo ambapo Wananchi wamelalamikia changamoto ya barabara ya kuelekea katika kituo hicho pamoja na kutokuwepo kwa daktari wa upasuaji.
Akitoa agizo hilo kwa Meneja huyo wa TARURA, Chongolo amemtaka hadi kesho Mei 28, 2023 barabara hiyo ya Kilomita moja iwe imeanza kutengenezwa.
Katika hatua nyingine Chongolo amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Iringa, Halima Dendego kuhakikisha hadi kesho kituo hicho cha afya cha Ifingo kinakuwa na Daktari anayeweza kutoa matibabu ya upasuaji, ili Wananchi wawe na uhakika wa matibabu wanapofika katika kituo hicho.
Chongolo yupo mkoani Iringa kwa ziara ya siku saba, ambayo ina lengo la kukagua uhai wa chama na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 -2023.