Chongolo aeleza mkakati wa kutatua changamoto ya mbolea

0
241

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amefafanua, sababu za mbolea kupanda bei ikiwa ni kilio cha wakulima hasa katika mikoa inayozalisha mazao ya kilimo kwa wingi, huku akitaja UVIKO-19 kuwa ndio chanzo kikuu cha gharama hiyo kupanda.

Chongolo amesema hayo wakati akihutubia wananchi, viongozi wa chama na serikali ngazi za wilaya na mkoa, katika mkutano wa mapokezi kata ya Pongwe wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi ambapo Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ipo mkoani humo kwa ziara ya siku mbili kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM na kuhimiza uhai wa chama ngazi ya mashina.

“Wote mnajua kuna kitu kinaitwa Korona, ugonjwa huu umetokea huko kwa wenzetu China na mataifa mengine makubwa, ambapo ulipoanzia ndipo walipo wazalishaji wakubwa wa mbolea na ililazimisha watu hao wajifungie ndani, ingawa huku kwetu tuliendelea na shughuli wakati wenzetu walikuwa wamejifungia na hakukuwa na mtu aliyekuwa anazalisha. Matokea yake tukatumia mbolea yote iliyokuwa kwenye akiba, na mashamba yao walipofungua wakaitumia yote na kusababisha uhaba mkubwa na bei kupanda,” Chongolo amefafanua

Hata hivyo katika jitihada za kuhakikisha changamoto hiyo haijirudii tena serikali imeweka mkakati wa kuzalisha mbolea hapa nyumbani kwa kiwanda kitakachojengwa Dodoma.