Cheyo, Mbatia, Shibuda na Rostam wakutana na Rais

0
1615

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na wanasiasa John Cheyo, James Mbatia, John Shibuda pamoja na mfanyabiashara Rostam Aziz Ikulu jijini Dar es salaam.

Baada ya mazungumzo hayo, Rostam Aziz amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi bora kwa kuwa amekuwa akitengeneza misingi imara ya uchumi unaokua kwa uhakika zaidi kwa kujenga miundombinu ya barabara, reli na bandari ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi na kuzalisha ajira.

Ameongeza kuwa anaunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuwaletea Watanzania maendeleo, huku akibainisha kuwa jukumu la wafanyabiashara ni kutumia fursa nyingi zilizopo katika viwanda, ujenzi na nyinginezo.

“Tunamuunga mkono Rais kwa kuhakikisha Watanzania tunawekeza katika nchi yetu, kukuza uchumi wetu, hilo ndilo la msingi kwa sisi wafanyabiashara” amesema Rostam Aziz.

Naye mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, – James Mbatia amesema kuwa katika kutekeleza malengo 17 ya dunia, Tanzania inafanya vizuri katika lengo la elimu ambalo linazungumzia elimu bora na shirikishi.

Mbatia amesisitiza kuwa Watanzania wote wana kila sababu ya kuendelea kuijenga nchi yao kwa mawazo ya pamoja yanayozingatia ujumbe uliomo katika wimbo wa Taifa unaosisitiza hekima, umoja na amani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda amesema kuwa amekutana na Rais Magufuli ili kumpongeza kwa uamuzi mzuri alioufanya kutatua tatizo la soko la korosho na kumhakikishia kuwa vyama vya siasa vinamuunga mkono kwa uongozi mzuri unaolenga kurekebisha dosari za mmomonyoko wa maadili ndani ya serikali na taasisi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa.

“Katika miaka mitatu, Rais Magufuli amerejesha sifa ya utaifa wetu ya kuwa nchi ya kuaminika na kusadikika na amekweza ari ya uhuru na kujitegemea, tulikuwa na hali duni na dumavu ya maendeleo na ustawi wa jamii, tulikuwa na hali ambayo maendeleo yetu hayawiani na maliasili tulizonazo na rasilimali tulizonazo” amesisitiza Shibuda.

John Cheyo ni Mwenyekiti wa Chama Cha UDP ambaye amempongeza Rais Magufuli kwa msimamo na ujasiri aliouonesha katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake na ametaka Watanzania wajivunie kuwa na Rais ambaye ameonesha dhamira njema ya kufikia nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Sisi Watanzania ni lazima tujivunie Rais tuliyenae, ni Rais anayetoa maamuzi, hata kama yatakuwa magumu kiasi gani, akiamua kusema tunakwenda kujenga Stieglers’ Gorge tutakwenda, akiamua kuwa tunakwenda kujenga standard gauge tunakwenda, akiamua watoto watasoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari inafanyika, na katika miaka mitatu hii imedhihirika kuwa maamuzi yake yanalisaidia Taifa sana” amesema Cheyo.