Chato: Vilio vyatawala mwili wa Dkt. Magufuli ukiwasili nyumbani

0
338

Mamia ya wakazi wa Wilaya ya Chato mkoani Geita wamejitokeza kupokea mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli, huku vilio vya huzuni vikitawala.

Wakazi hao wakiwa mithili ya mtoto aliyeondokewa na baba, wamempokea mpendwa wao lakini kwa siku ya leo akiwa amelazwa kwenye jeneza, huku wakimuita lakini hawasikii tofauti na siku nyingine alipokuwa akirudi nyumbani.

Mara nyingine walizoea akija hapa kwa ajili ya mapumziko mafupi na kisha anarejea kwenye majukumu yake, lakini leo amepumzika moja kwa moja, ni huzuni kwa wakazi hao na Watanzania kwa ujumla.

Miongoni mwa mabango yaliyoukaribisha mwili wa shujaa huyo wa Afrika yanaeleza kuwa yeye ni muadilifu, mnyenyekevu, jeshi, msikivu na kwamba watamkumbuka daima.

Baba umetutoka, kwaheri Baba ni baadhi ya maneno yaliyotumiwa na Wakazi hao kuonesha hisia za uchungu kuondokewa na mwanamapinduzi wao.

Wakazi hao wa Chato watauaga mwili huo kesho Machi 25, 2021 na utawekwa kwenye nyumba yake ya milele Machi 26, 2021 nyumbani kwake Chato mkoani Geita.