Chanzo cha ajali ya mwendokasi ni uzembe

0
254

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema chanzo cha ajali iliyohusisha basi la ‘mwendokasi’ na gari dogo aina ya RAV 4 ni uzembe wa dereva wa gari hilo dogo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa gari hilo dogo
kukatisha barabara ya mwendokasi bila kuchukua tahadhari wakati huo mwendokasi ikiwa kwenye barabara yake.

Akitoa taarifa rasmi ya ajali hiyo iliyotokea hapo jana katika eneo la Kisutu, Kamanda Muliro amewaambia waandishi wa habari kuwa majeruhi ambao wapo hospitalini mpaka kufikia leo ni wanne.

Amesema kati ya majeruhi hao wanne, watatu ni wale waliokuwa kwenye gari dogo lililosababisha ajali ambao ni dereva na abiria wake wawili na wamelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, majeruhi mwingine ni mtembea kwa miguu ambaye ameonekana kwenye picha za video akigongwa na mwendokasi, ambaye amelazwa kwenye Taasisi ya Mifupa (MOI) chumba cha uangalizi maalum.