Tanzania imepokea dozi 115,200 aina ya JANSSEN za chanjo dhidi ya UVIKO – 19, ikiwa ni moja ya mikakati ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa huo.
Akipokea chanjo hizo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mkoani Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema chanjo hiyo ni ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji kupitia mpango wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kupambana na maambukizi ya UVIKO – 19 (Covax Facility).
Hii ni awamu ya tatu kwa chanjo aina ya JANSSEN kupokelewa nchini kupitia mpango wa COVAX.
Aidha Waziri Gwajima amesema chanjo dhidi ya UVIKO – 19 zipo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali, na kutoa rai kwa wale ambao bado hawajapata chanjo kwenda kupata chanjo hiyo.