Chaneli za Tanzania sasa ndani ya DStv

0
225

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, ametangaza kurejeshwa kwa chaneli za Tanzania (Local Channels) kwenye mfumo wa matangazo wa moja kwa moja wa Satelite (DTH) kuanzia wiki hii.

Waziri Nape ameyasema hayo leo 31 Januari 2022, alipotembelea ofisi za kampuni ya MultiChoice Tanzania (DStv) ikiwa ni sehemu ya ziara zake kwa wadau wa wizara anayoingoza.

Waziri Nape amesema Serikali imefanya mapitio ya kanuni za sekta ya utangazaji nchini na kwa mujibu wa marekebisho hayo sasa visimbuzi vyote vya antena (DTT) vile vya dish (DTH) vitaruhusiwa kubeba chaneli hizo.

Amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya habari popote walipo bila usumbufu na kwa njia wanayoipendelea wao wenyewe.

“Tumefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya habari na tumefanikiwa kufanya marekebisho kwenye kanuni kadhaa na lengo la haya yote ni kuhakikisha kuwa Mtanzania popote alipo anapata habari, elimu na burudani kupitia mifumo na mitandao mbalimbali bila vikwazo” amesema Waziri Nape.

Mapema mwaka 2018 chaneli za ndani ziliondolewa kwenye visimbuzi vya dishi kitendo kilichosababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kwani wengi walisindwa kuzipata chaneli hizo kama ITV, EATV, Clouds TV, Channel Ten, Star TV na hata chaneli za dini kama vile Imaan TV, Upendo TV na nyinginezo.

Akimkaribisha Waziri ofisini kwake, Mwenyekiti wa Bodi ya MultiChoice Tanzania Balozi Ami Mpungwe amesema kitendo cha Waziri kuzuru wadau siku chache baada ya uteuzi wake ni dalili njema kwani itamuwezesha kufahamu maendeleo na changamoto za wadau na pia kujadiliana njia bora za kushirikiana katika kukuza sekta ya Habari na Mawasiliano hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso amempongeza waziri na wizara kwa ujumla kwa kukamilisha zoezi la mapitio ya kanunu mbalimbali za sekta ya utangazaji zilizoruhusu kuonyeshwa kwa chaneli za ndani kwenye mifumo mingi zaidi.

“Tumefurahishwa na mabadiliko haya ambayo kimsingi yanajibu mahitaji ya wananchi wetu wengi ambao kila uchao walikuwa wakiomba kuruhusiwa kwa chaneli za ndani katika visimbuzi vya DStv na vingine. Tunaamini hii ni hatua muhimu kwana itawarahisishia zaidi wananchi kupata huduma za matangazo kwa urahisi” alisema Jacqueline.

Mkurugenzi huyo amesema DStv itatekeleza agizo la waziri kwa kuhakikisha kuwa wanaharakisha mchakato wa kuzibeba chaneli hizo ndani ya muda mfupi.