Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe, umesema wameridhishwa na mchakato wa uchukuaji fomu za wagombea.
Akizungumza na TBC, Katibu wa chama hicho Wilaya ya Songwe, Octavian Ululu, amesema mchakato huo ulikuwa huru na uliozingatia demokrasia kwa wagombea wa vyama vyote bila kujali itikadi za vyama vya siasa.
Octavian pia amempongeza Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Songwe, CPA Cessilia Kavishe, kwa kuwa na mwitikio wa haraka pindi changamoto zinapojitokeza.
“Kwakweli nampongeza sana Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Wilaya hii; amekuwa na mwitikio sana pale tunapowasilisha changamoto zetu na zinatatuliwa kwa wakati,” amesema Octavian.
Kiongozi huyo wa upinzani ametoa wito kwa wananchi na viongozi kuendelea kufanya siasa za kistaarabu ili kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa kufuata kanuni na hivyo kuwa huru na wa haki.