CCM yaagiza kiwanda cha Mponde kifunguliwe

0
252

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo, ameagiza kufunguliwa kwa kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo mkoani Tanga ifikapo mwezi Septemba mwaka huu, ili kuwanusuru wakulima walioacha kupeleka chai kiwandani hapo kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Chongolo ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa eneo la Soni wilayani Lushoto, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu mkoani Tanga.

Amesema lengo la serikali ni kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, ndio maana inaongeza nguvu kwenye eneo la uwekezaji ikiwemo kufufua viwanda vya ndani.

Kiwanda cha chai cha Mponde kinategemewa na wakulima zaidi ya 1,500 waliokuwa wakipeleka chai kiwandani hapo kutoka wilaya za Lushoto na Korogwe.

Aidha Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa amewataka wazazi na walezi nchini kuwasomesha watoto wa kike badala ya kuwaozesha.

Amesema kuwaozesha watoto mapema ni kuwakosesha fursa za elimu.