Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema ukusanyaji wa mapato ya ndani yaliyowasilishwa na mamlaka ya Serikali za mitaa 184 yamezidi makadirio ya awali kwa asilimia mbili.
Akiwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan taarifa ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, Kichere amesema makusanyo ni shilingi bilioni 891.84, sawa na asilimia 102 huku makadirio yakiwa ni shilingi bilioni 873.9.
Ameongeza kuwa mbali na mafanikio hayo, yapo mapungufu ikiwemo ufuatiliaji duni wa fedha uliosababisha kutowasilishwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 11.07 benki kwa mamlaka 98 za serikali za mitaa.
Kichere ametoa wito kwa wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha fedha hizo zinawasilishwa benki kwa mujibu wa sheria na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.