Byakanwa aagiza ujenzi wa gati namba mbili uharakishwe

0
209

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, – Gelasius Byakanwa ameziagiza kampuni za China Railways Major Bridges Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) na China Railways Construction Engineering Group (CRCEG) zinazojenga gati namba mbili katika bandari ya Mtwara kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.

Byakanwa ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi huo na kutoridhishwa na maendeleo yake ambao mpaka sasa umefikia asilimia 68.

Ujenzi wa gati namba mbili katika bandari hiyo ya Mtwara ulianza mwaka 2017 na kutakiwa kukamilika mwezi Februari mwaka 2019, lakini ilishindikana na hivyo kampuni hizo kuongezewa muda.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa wa Mtwara, kwa sasa ujenzi huo unatakiwa kukamilika Julai 31 mwaka huu.

Hadi kukamilika kwake, ujenzi huo wa gati namba mbili katika bandari ya Mtwara unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 137.