Buriani Shujaa wa Afrika, Dkt. Magufuli

0
338

Leo Aprili 6, 2021 ni siku ya mwisho ya maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kilichotokea Machi 17 katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

Akitangaza taarifa za kifo hicho zilizowashtua Watanzania wengi, Rais wa Tanzania (akiwa Makamu wa Rais wakati huo), Samia Suluhu Hassan alisema kuwa Dkt. Magufuli alifariki dunia kutokana na maradhi ya moyo, ugonjwa ambao umekuwa ukimsumbua kwa zaidi ya miaka 10.

Kufuatia msiba huo, Serikali ilitangaza siku 21 za maombolezo kuanzia Machi 17, siku zinazoisha hii leo ambapo bendera zote zimekuwa zikipepea nusu mlingoti.

Tukio la kuagwa na kuzikwa kwa Dkt. Magufuli liliudhihirishia ulimwengu namna gani Shujaa huyo wa Afrika alivyopendwa na watu wake kutokana na yale mengi aliyoyafanya ambayo yaligusa kwa namna mbalimbali maisha ya Watanzania wote.

Jeshi, Jiwe, Chuma, Baba, Mtetezi na Shujaa ni baadhi tu ya majina waliyokuwa wakiyatamka Wananchi wakati mwili wa Dkt. Magufuli ulipopitishwa katika viunga vya Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Geita.

Kwa miaka mitano na miezi minne aliyohudumu kama Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli aliweza kufanya mabadiliko makubwa kuanzia kwenye nidhamu ya ya Watumishi, matumizi ya fedha hadi kwenye ujenzi wa miundombinu.

Dkt. Magufuli alifanikiwa kusimamia ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP), Daraja la Juu la Kijazi, Daraja la Juu la Mfugale, daraja la Kigongo-Busisi, upanuzi wa viwanja wa ndege, uboreshaji wa sekta ya afya na elimu bure.

Dkt. Magufuli ambaye alizikwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita Machi 26, 2021 ameacha mjane na watoto saba.