Bunge limepitisha muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali namba 2 wa mwaka 2022, ambapo mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Elieza Feleshi amewasilisha mabadiliko katika baadhi ya maeneo kwenye sheria ya udhibiti wa dawa za kulevya.
Sheria nyingine ambazo zimefanyiwa marekebisho ni pamoja na sheria ya kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu na Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma.
Akiwasilisha Muswada huo bungeni jijini Dodoma, Dkt. Feleshi amesema serikali inafanya mabadiliko ya kifungu namba 11(2) b katika sheria ya maadili ya viongozi wa umma na kuondoa kifungu kilichokuwa kikiwataka viongozi kutaja mali zao ikiwa ni pamoja na vitu vya ndani.
Mabadiliko hayo pia yamehusisha sheria ya kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu fungu la 432 na sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya fungu namba 95.
Vifungu vilivyofanyiwa marekebisho katika sheria ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya ni pamoja na kifungu cha 4, 5, 6, 7, 8A na 13 kwa lengo la kuongeza adhabu zilizoainishwa katika vifungu hivyo.
Wakichangia mjadala kuhusiana na mabadiliko ya sheria hizo baadhi ya wabunge wameitaka serikali kuhakikisha inasimamia mabadiliko hayo, ili kudhibiti biashara haramu za kusafirisha binadamu na zile za dawa za kulevya.