Bunge lapitisha bajeti ya trilioni 44 kwa kishindo

0
360
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba akihitimisha hoja ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 bungeni jijini Dodoma.

Bunge la Tanzania leo limepitisha bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka 2023/24 ya shilingi Trilioni 44.39, ambapo wabunge 354 sawa na asilimia 95 wamepiga kura za ndio, wabunge 20 wamepiga kura za kutoamua na hakuna mbunge ambaye ameikataa.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo pamoja na Muswada wa Fedha wa mwaka 2023/24 kunatoa nafasi kwa Serikali kuanza kutekeleza bajeti hiyo kuanzia mwaka wa fedha Julai Mosi mwaka huu.

Lengo kuu la bajeti ya mwaka ujao ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha sekta za uzalishaji ili kuboresha hali ya maisha.

Wakati wa kujadili bajjeti hiyo mambo kadhaa yaliibua mjadala mkali ikiwa ni pamoja na tozo ya shilingi 100 kwa kila lita moja ya dizeli na petroli ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwiguli Nchemba, fedha zitakazokusanywa zitatunisha mfuko wa Serikali na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kuhusu suala la tozo ya shilingi 1,000 kwa kila mfuko wa saruji inayotoka nje na kuzalishwa nchini, Dkt. Mwigulu amesema kuwa fedha zitakazokusanywa zitatumika kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati wanaochaguliwa na Serikali kusoma fani za kipaumbele ambazo ni sayansi, afya, ufundi na ualimu.

Wakati huo huo, Serikali imepongezwa kwa hatua kadhaa ilizochukua ikiwa ni pamoja na kusitisha utaratibu wa kufungia biashara, badala yake hatua kuchukuliwa dhidi ya mwenye biashara, kuweka mazingira mazuri ya kukuza biashara na uwekezaji, kufuta ada kwa vyuo vitatu vya ufundi, kutoa mikopo kwa elimu ya vyuo vya kati, kupunguza kodi kwenye malighafi hasa zinazogusa biashara za wajasiriamali pamoja na kufanyia marekebisho sheria mbalimbali ili kuondoa mwingiliano wa majukumu ya taasisi zake.