Bunge lapitisha azimio la kuridhia ushirikiano Tanzania na Dubai

0
563

Bunge la Tanzania limepitisha Azimio la Kuridhia Mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii wa Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari Tanzania.

Azimio hilo limepitishwa leo baada ya wabunge kutumia takribani saa tano kuchangia azimio hilo ambalo kwa takribani wiki moja limeibua mjadala mkubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Akitoa hoja ya Serikali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ametolea ufafanuzi hoja mbalimbali akisema kuwa hadi sasa hakuna mkataba wowote uliosainiwa kuhusu uendelezaji wa bandari, na kwamba baada ya azimio hilo kupitishwa, Serikali itakuwa na miezi 12 ya kufanya majadiliano na Serikali ya Dubai na endapo muda huo ukiisha bila mwafaka kufikiwa, Serikali inaweza kutafuta wawekezaji wengine.

Prof. Mbarawa amesema walifikia mwafaka wa kuichagua DP World kati ya kampuni nyingi zilizoonesha nia ya kuwekeza katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na uwezo na uzoefu wake mkubwa hasa katika kuhudumia bandari za Afrika.

Miongoni mwa mafanikio ambayo Tanzania inatarajia  kupata kutokana na uwekezaji huo ni pamoja na kupunguza muda wa meli nangani kutoka siku siku 5 hadi saa 24, kupunguza muda wa ushushaji meli kutoka siku 4.2 hadi siku 2, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa 12 hadi saa 1 na kuongeza ajira kwa Watanzania kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi 71,907 mwaka 2032/33.

Mbali na wabunge waliounga mkono azimio hilo, baadhi ya wabunge wamepinga azimio hilo wakisema lina kasoro na kwa sababu azimio hilo ndio litakuwa msingi wa mikataba itakayoingiwa, wameonesha hofu kuwa mikataba hiyo huenda ikawa na kasoro.