BOT yatakiwa kusaidia kuboresha sekta ya kilimo

0
273

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, -Doto James ameishauri Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kukutana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuweka mikakati ya namna ya kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza tija katika sekta hiyo inayotegemewa na idadi kubwa ya Watanzania.

James ametoa ushauri huo wakati wa kikao kati ya Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Menejimenti ya Benki Kuu ya Tanzania, kikao kilichojadili masuala mbalimbali yanayogusa majukumu ya Benki Kuu.

Amesema kuwa kilimo ambacho kina ajiri karibu asilimia 70 ya Watanzania, bado hakijafanya vizuri na kubainisha kuwa Benki Kuu inayo nafasi kubwa ya kutoa mawazo na mchango wake wa kitaalamu ili kilimo na ufugaji viwe na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Gavana wa Benki Kuu Dkt Yamungu Kayandabila amesema kuwa, nchi karibu zote zilizoendelea duniani zimefanikiwa kufikia hatua hiyo kutokana na sekta ya kilimo ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa malighafi za viwanda.

Ameahidi kuwa Benki Kuu iko tayari kuratibu mkutano na Wizara ya Kilimo, Mifugo, na ile ya Viwanda na Biashara ili kutafuta njia za kuinua kilimo ikiwemo uongezaji wa thamani ya mazao na kuinua kiwango cha bidhaa za kilimo zinazouzwa nje ya nchi.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Gavana wa Benki Kuu Profesa Florens Luoga, aliyeongoza ujumbe wa Benki Kuu ya Tanzania.