Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii nchini (TTB), imempa Muingereza Nick Reynald maarufu kama Bongozozo ubalozi wa utalii wa Tanzania nchini Uingereza.
Akizungumza katika hafla ya kumkabidhi barua ya utambuzi kwa ajili ya kazi, Meneja Masoko wa TTB, Geofrey Meena amesema kuwa, Nick Reynald aliyezaliwa Zimbabwe na kuishi Tanzania kwa miaka 18 atakuwa balozi mzuri kwa utalii wa Tanzania kwa sababu anajua maeneo mengi ya utalii.
“Nick Reynald ‘Bongozozo’ ameishi hapa nchini kwa miaka mingi kuanzia mwaka 1998, hivyo anauelewa utalii wa Tanzania, amekuwa maarufu sana hapa nchini kutokana na mapenzi makubwa kwa Tanzania ambayo yemejidhihirisha katika nyanja nyingi ikiwemo ushabiki wa mpira kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) pamoja na wachezaji akiwemo Mbwana Samatta anayekipiga kunako klabu ya mpira ya Aston Villa ya Uingireza,” amesema Geofrey Meena.
TTB imedhamiria kukuza utalii kwa kuongeza watalii kutoka Uingereza kwa kuwa nchi hiyo ni ya pili kwa kuleta watalii wengi nchini ikitanguliwa na Marekani. Takwimu za utalii mwaka 2018 zinaonesha kuwa watalii kutoka Uingereza walikuwa 77,199 huku Marekani ikileta watalii 94,876.
Kwa upande wake Bongozozo amesema kuwa yeye atakuwa balozi mzuri katika kutangaza mazuri ya Tanzania na utalii wake duniani kote kupitia mitandao yake ya kijamii ili kuleta watalii nchini.
“Nikizunguka duniani kote kupitia mitandao yangu ya kijamii nitawaambia kuwa Tanzania ni nchi yenye watu wakarimu sana, nitazidi kuipeperusha bendera ya Tanzania na nitawaeleza sehemu za kitalii zilizoko Tanzania, kwa hiyo nimekubali kuitangaza Tanzania kwa watalii wengi duniani,” amesema Bongozozo.