Bonanza la bunge lafana

0
206

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasisitiza wabunge na wananchi wengine kushiriki katika michezo, ili kuipa miili yao nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya kikazi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo aliposhiriki bonanza lililoandaliwa na bunge na kufanyika katika viwanja vya shule ya msingi na sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.

“Michezo kwetu sisi wabunge ni muhimu zaidi kwa sababu inatufanya tuwe na afya bora zaidi na pia michezo inasaidia watu kukutana pamoja na kuimarisha undugu, kujenga urafiki pamoja na kukuza vipaji.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson kwa ubunifu wa kuanzisha Bunge Bonanza ambalo litakuwa linafanyika mara kwa mara.

Bonanza hilo limeshirikisha wabunge, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Watumishi wa Bunge pamoja na maafisa wa serikali.

Kwa upande wake, Spika Tulia amesema Bunge Bonanza litakuwa linafanyika mara nne kwa mwaka, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi umuhimu wa kushiriki katika kufanya mazoezi ili jamii iweze kuwa na afya bora zaidi.