BOA yashauriwa kupanua huduma zake nchini

0
212

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameishauri Benki ya Afrika (BOA) kuendelea kupanua wigo wa huduma za benki hiyo nchini, ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi hasa katika sekta  za elimu, kilimo, mifugo na madini.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye anaendelea na ziara yake nchini Morocco ametoa ushauri huo jijini Rabat, wakati wa mazungumzo yake na Rais wa BOA Othman Benjelloun.

Ameishukuru Benki hiyo ya Afrika kwa jitihada zake za kuendelea kuisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, uwepo wa benki hiyo ya Afrika nchini Tanzania umewawezesha Wananchi kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.

 
Ameahidi kuandaa utaratibu wa kuukutanisha uongozi wa benki hiyo na sekta binafsi nchini Tanzania, ili kuona namna watakavyoweza kushirikiana katika kuwahudumia Watanzania.
 
Kwa upande wake, Benjelloun amesema lengo la BOA ni kuendelea kukuza uwekezaji wake  nchini Tanzania.

“Sisi tupo tayari kuwekeza katika maeneo mbayo Viongozi wa Taifa la Tanzania watatushauri, lengo likiwa ni kutoa mchango wetu katika kujenga uchumi.” amesema Rais huyo wa BOA Othman Benjelloun.