Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza menejimenti na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa ubora wa huduma.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stansilaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya huduma za kibingwa na bingwa bobezi zinazotolewa katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma.
“Hongereni kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuwahudumia Watanzania lakini pia mkurugenzi usisite kutuma vijana wako kuendelea kujifunza ili Tanzania tuzidi kuwa kivutio cha tiba utalii Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” amesema Nyongo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika ameishukuru Serikali kwa uwekezaji ilioufanya katika hospitali hiyo hususani kwenye vifaa tiba na vitendanishi, kusomesha wataalamu na upatikanaji wa dawa kwa wakati.