Bima ya afya kwa wote mkombozi kwa wagonjwa wa moyo

0
413

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema, Bima ya Afya kwa wote itawasaidia wananchi wengi ambao wanashindwa kumudu gharama za matibabu ya moyo.

Dkt. Kisenge ameyasema hayo katika mahojiano na TBC kwenye kipindi cha Jambo Tanzania.

Amesema matibabu ya moyo yana gharama kubwa, na ili mgonjwa afanyiwe upasuaji mkubwa wa mirija ya moyo atahitaji zaidi ya shilingi milioni 15 na ikiwa atakwenda kupata matibabu hayo nje ya nchi atahitajika kuwa na zaidi ya shilingi milioni 30.

Kwa mujibu wa
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa JKCI, endapo mwananchi atakuwa na Bima ya Afya itamsaidia kupata huduma hiyo bila kuchelewa.

“Tunapata shida kwenye taasisi ya moyo kwa sababu wananchi wengi hawana uwezo, gharama ya kuanzia milioni 8 hadi 15 ni ngumu sana ndio sababu serikali ikaona kila mwananchi sasa ni vizuri awe na bima ya afya na kama bunge litapitisha mwakani basi wananchi wote wataipata hii bima ya afya.” amesema Dkt. Kisenge

Amesema ili kuipata Bima hiyo ya Afya kwa wote, familia italazimika kuchangia kiasi cha fedha akitolea mfano kwa familia yenye watu sita itachangia shilingi 384,000 kwa mwaka.