Bilioni 54 kujenga mradi wa maji Ruangwa/Nachingwe

0
141

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imetoa shilingi bilioni 54 kwa ajili ya kugharamia mradi wa maji wa Chiuwe utakaohudumia wilaya za Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wananchi katika vijiji vya Mchenganyumba, Mbecha na Chimbila ‘B’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya ya Ruangwa.

Amesema maeneo mengi ya wilaya ya Ruangwa maji yake ni ya chumvi, hivyo serikali ilifanya utafiti na kubaini kuwa chanzo cha maji cha Chiuwe maji yake hayana chumvi na ni ya kutosha kuweza kuhudumia vijiji vya wilaya hiyo na wilaya jirani ya Nachingwea.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kitakachowezesha kutekelezwa kwa mradi huo ambao kukamilika kwake kutamaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama wilayani Ruangwa.
 
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wa wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Lawrence Mapunda amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza itahusisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 21 vya wilaya ya Nachingwea.

Amesema ujenzi wa mradi huo ambao unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 utakamilika mwaka wa fedha wa 2025/2026.