Bilioni 50 kumaliza changamoto ya maji Tanga

0
146

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amesema uchumi wa Mkoa wa Tanga umekua kutoka shilingi trilioni 4 hadi trilioni 7.9 ndani ya kipindi cha miaka minne kutokana na mazingira mazuri ambayo serikali imeendelea kuyaweka kupitia uwekezaji.
Kindamba alikuwa akitoa salamu za mkoa katika Uzinduzi wa Hati Fungani ya Kijani ya Miundombinu ya Maji yenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni 50 ambayo imeidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

“Kuzinduliwa kwa hati fungani hii kutachagiza ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Tanga ambao kila uchao umeendelea kushika kasi na mradi huu ambao utauzindua leo unaandika historia Afrika Mashariki na utasadia kupatikana kwa maji ya uhakika,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga-UWASA), Geofrey Hilly amesema ifikapo 2025 Jiji la Tanga litakuwa na uhakika wa kupata maji saa 24 kupitia mradi huo na kuondoa kero kwa wananchi ambao wamekuwa wakihangaika kupata maji safi na salama.